Katika kuadhimisha siku ya kimataifa ya demokrasia na maudhui, yanayoangazia uhuru wa vyombo vya Habari hii leo Septemba 15, 2022 Katibu Mkuu wa Umoja wa Mataifa, Antonio Guterres amesema bado demokrasia inazidi kurudi nyuma Duniani kote.
Guterres, ameyasema hii leo jijini Geneva nchini Uswisi na kuongeza kuwa matukio ya waaandishi wa Habari kunyanyaswa na kuteseka yanaongezeka, ikiwemo kuwekwa vizuizini, kukumbwa na unyanyasaji wa kimwili na hata kuuawa.
Amesema, “mateso haya yanafanyika pia mtandaoni ambako wamekuwa wakifuatiliwa na kushambuliwa kwa maneno hususani wanawake na kuonya kuwa bila vyombo huru vya Habari, demokrasia haiwezi kuendelea, na kwamba bila uhuru wa kujieleza hakuna uhuru.”
Guterres ameongeza kuwa, taarifa zinazoenesha hata uhuru wa wananchi kuzungumza unazidi kupungua, na mkanganyiko wa taarifa potofu umezidi kusambaa miongoni mwa jamii, huku ubaguzi nao kudhoofisha taasisi za kidemokrasia zinazopigania uhuru wake.
Ameongeza kuwa, “Sasa ni wakati wa kuongeza tahadhari. Sasa ni wakati wa kuthibitisha kwamba demokrasia, maendeleo na haki za binadamu vinategemeana na vinaimarishana. Sasa ni wakati wa kutetea kanuni za kidemokrasia za usawa, ushirikishwaji na mshikamano.”
Mkuu huyo wa umoja wa Mataifa, amehitimisha ujumbe wake wa siku ya leo kwa kusema katika siku ya Demokrasia na kila siku, ni lazima kuunganisha nguvu kwa pamoja ili kupata uhuru na kulinda haki za watu wote, ulimwenguni.