Kutungwa kwa sheria ya Habari ya mwaka 2016, kulilenga kuipunguza Serikali uendeshaji wa vyombo vya habari, njia ambayo itapunguza madaraka kwa Mkurugenzi wa Idara ya Habari Maelezo, sambamba na Wanahabari kujisimamia katika majukumu yao.

Waziri wa Habari, Mawasiliano na Teknolojia ya Habari, Nape Nnauye ameyasema hayo na kudai kuwa Mkurugenzi wa Idara ya Habari (MAELEZO), ndiye mwakilishi wa Serikali katika kusimamia vyombo vya habari, na kwamba wanataka madaraka yake yapungue kadri inavyowezekana.

Amesema, sehemu kubwa ya usimamizi wa vyombo vya habari inatakiwa ibaki kwa wanataaluma, tofauti na sheria ya habari ya mwaka 1976 ambayo iliingiza mikono mingi ya usimamiaji wa vyombo vya habari.

Nape ambaye alikuwa akihojiwa na kipindi cha Dira ya Dunia cha BBC, amesema, “sheria hii tukatamani ipunguze, na namna ya kupunguza ilikuwa ni pamoja na kuunda Baraza Huru la Wanahabari ili yale ya kitaaluma wayamalize huko.”

Aidha ameongeza kuwa, waandishi wa habari kama wanataaluma wengine wakiwemo wanasheria wanatakiwa kujisimami wenyewe, na kuweza kuendesha mambo yao bila kuwa na vikwazo.

Ameongeza kuwa, “Sisi kama serikali tubaki na vitu vichache sana vinavyolinda nchi, usalama na afya ya jamii lakini mengine yafanywe na wanahabari wenyewe na inawezekana maana madaktari wamefanya imewezekana, wanasheria wamefanya imewezekana.”

Mdee na wenzake 18 watinga Mahakamani
Msiri wa Mwakinyo afunguka pambano la England