Wizara ya Afya imeendelea na mpango mkakati wa kusambaza kingatiba kwa wananchi wote ili kudhibiti magonjwa yaliyokuwa hayapewi kipaumbele ikiwemo matende na mabusha, vikope, kichocho, minyoo na Usubi

Mkurugenzi Mkuu NIMR Prof. Yunus Mgaya amesema lengo kuu la mpango huo ni kutokomeza kabisa magonjwa hayo kule ambako yanaendelea kutokea ambapo hadi kufikia sasa wilaya 9 zimebaki ili kutokomeza kabisa kwa upande wa ugonjwa wa matende na mabusha.

“Tumeweka nguvu kubwa kabisa katika kuhakikisha kwamba maeneo yote ambayo yameathirika na magonjwa haya, wananchi wanapewa kingatiba kwa ujumla”

Aidha, Prof. Mgaya amesema mpaka kufikia mwaka 2030 wataweza kutokomeza magonjwa kwa kiasi cha kutangaza magonjwa hayo siyo tena mzigo katika sekta wa Afya nchini Tanzania.

“Mkakati wa kutoa kingatiba umewezesha kupunguza magonjwa katika sehemu mbalimbali za nchi, wilaya nyingi ambazo zilikuwa na matatizo haya sasa hivi hakuna tena zimebaki wilaya chache, kwa mfano ugonjwa wa matende na mabusha tumebaki na wilaya 9, na tunaamini tukiendelea hivi ikifika mwaka 2030 tunaweza tukawa tumepunguza magonjwa kwa kiasi cha kutangaza kwamba Tanzania magonjwa haya siyo tena mzigo katika mfumo wa Afya,” amesema Prof. Mgaya.

Wilaya ambazo bado Magonjwa haya yapo ni pamoja na Ilala, Kinondon, Temeke, Mtama, Lindi, Mafia, Kilwa, Pangani na Mtwara Mikindani.

Pia Prof. Mgaya ameendelea kuwasisitiza wananchi wote kufuata maelekezo yote yanayotolewa na wataalamu wa Afya na inapofikia wakati wa kutoa kinga tiba zinazosambazwa wasiache kumeza kingatiba.

Kwa upande wake Mwakilishi wa taasisi ya utafiti wa kimataifa (RTI) kutoka Marekani, Dkt. Upendo Mwingira amesema wamekua wakifanya tathmini kwa kushirikiana na wizara ya afya na wadau kutoka NIMR ili kuweza kujua kingatiba wanazozitoa zina matokeo gani.

“Idadi ya wilaya ambazo zimekuwa zikipewa kingatiba zimeshuka kutoka 119 mpaka wilaya 9 ambapo wilaya 110 zote zimekuwa hazina hatari ya maambukizi ya matende na mabusha nchini,” amesema Dkt. Mwingira.

Dkt. Mwingira aliongeza kuwa kutokana na Shirika hilo kujikita katika kuboresha mifumo ya Afya katika kuangalia jinsi gani baada ya kugawa kingatiba kwa jamii kuwa itaweza kuhakikisha magonjwa hayo hayarudi tena.

Hivyo, amesema kuna haja ya kuboresha mifumo ya kijamii, kuboresha ushirikishwaji wa jamii katika kuelewa na kufahamu jinsi gani njia mbalimbali za kudhibiti magonjwa zinavyoweza kutumika ili ifikapo mwaka 2030 Tanzania inatokomeza magonjwa haya.

Mkutano wa 10 wa kutengeneza mpango kazi wa mwaka 2022/23 wa Mpango wa Taifa wa kudhibiti magonjwa yaliyokuwa hayapewi kipaumbele, umefanyika Agosti 25, 2022.

Kocha Simba Queens amkingia kifua Opa Clement
TAWA yachangia sehemu ya Bil. 1.26 za Serengeti na Tembo