Kikosi cha Mabingwa wa Soka nchini Sudan Al Hilal kinatarajiwa kuwasili Dar es salaam-Tanzania keshokutwa Alhamis (Oktoba 06), tayari kwa mchezo wa Mkondo wa Kwanza wa Ligi ya Mabingwa Barani Afrika.
Mpambano huo wa Mzunguuko wa Kwanza wa Michuano hiyo umepangwa kupigwa Jumamosi (Oktoba 08), Uwanja wa Benjamin Mkapa jijini Dar es salaam.
Inaelezwa kuwa tayari baadhi ya viongozi wa Klabu hiyo yenye maskani yake mjini Khartoum-Sudan, wameshawasili jijini Dar es salaam tangu jana Jumatatu (Oktoba 03), wakitokea Lubumbashi-DR Congo.
Wachezaji pamoja na Benchi la Ufundi bado wapo Lubumbashi-DR Congo wakiendelea kujiweka fiti ambapo kwenye ziara yao hiyo nchini humo tayari wameshacheza mechi ya kirafiki dhidi ya Don Bosco siku ya Jumapili na kushushiwa kipigo cha mabao 3-1, ambapo wachezaji wa Don Bosco walivaa jezi za TP Mazembe katika mchezo huo.
Hata hivyo kikosi hicho leo Jumanne (Oktoba 04) asubuhi kimeendelea kujifua kikiwa chini ya kocha mkuu Florient Ibenge.
Ikumbukwe mabingwa hao wa Sudan walisonga mbele na kuingia kwenye hatua hii baada ya kuitoa St. George ya Ethiopia kwa bao la ugenini, ambapo kwenye mchezo wa kwanza wakiwa ugenini walifungwa mabao 2-1 kisha waliporudi nyumbani wakaibuka na ushindi wa bao 1-0.