Mtaalamu wa Umoja wa Mataifa wa masuala ya ualbino, Muluka-Anne Miti -Drummond ametoa wito wa kuchukuliwa hatua za haraka ili kukabiliana na mashambulizi dhidi ya watu wenye ualbino ikiwa ni pamoja na mauaji na ukeketaji, ambayo yanaongezeka wakati huu ambapo imani potofu na umaskini ukizidi kushamiri.

Kupitia taarifa iliyotolewa kwa waandishi wa habari jijini Geneva Uswisi, Mtaalamu huyo Huru wa Umoja wa Mataifa amesema imani potofu na ushirikina kwamba macho ya watu wenye ualbino yanaweza kuleta bahati nzuri na utajiri vimeanzisha mashambulizi yanayolenga zaidi watoto akitolea mfano eneo la kusini mwa Madagascar.

Mtaalumu huyo ambaye alifanya ziara ya siku 10 nchini Magadascar katika siku za hivi karibuni, amesema, “Watu wenye ualbino, katika maeneo hayo wamekuwa wakiishi kwa hofu ya kudumu na wengine kuamua kuwachukua watoto wao na kuwaacha katika vituo vya Polisi au maeneo mengine kwa ajili ya kupatiwa ulinzi.

Watoto wenye Ualbino. Picha na EU-Logos Athena.

Umoja wa Mataifa, umeishauri Serikali ya Madagascar kuanzisha kampeni nchi nzima za kuelimisha na kuongeza uelewa wa kukabiliana na imani potofu, imani za kishirikina na kutoelewa kuhusu ualbino sambamba na mataifa mengine ambayo nayo yanatakiwa kuiga mfano huo ili kuthibiti hali hiyo.

Taarifa za kati ya mwaka 2020 na mwaka 2022 kutoka vyombo vya usalama viliripoti takriban kesi 45 ambazo ni pamoja na utekaji nyara, ukeketaji na mauaji na mashambulizi ya mwaka 2022 yameongezeka maradufu ikilinganishwa na 2021. Ndani ya mwezi mmoja mashambulio manne yamerekodiwa ambayo waathiriwa ni pamoja na mtoto wa miezi tisa.

Katika ziara yake nchini Magadascar, Mtaalamu huyo alitembelea jamii maskini huko Fort Dauphin, Ambovombe na Amoboasary akielezea alicho shuhudia kwamba eneo la kusini limeathiriwa zaidi na mabadiliko ya tabianchi na limekumbwa na ukame, vimbunga, uhaba mkubwa wa chakula na ukosefu wa usalama unaosababishwa na wezi wa mifugo wanaojulikana kama dahalo.

Al Hilal kutua Dar es salaam Oktoba 06
12 wafariki katika shambulio, yupo Waziri wa Afya na Mkuu wa Wilaya