Ikiwa zimepita siku tatu, baada ya Jamhuri ya Kidemokrasia ya Watu wa Korea, DPRK kurusha kombora la masafa marefu kupitia anga la Japan, hii leo Baraza la Usalama la Umoja wa Mataifa, limekuwa na kikao kuhusu tukio hilo ambapo jamii ya kimataifa imetakiwa kuimarisha juhudi zake kutokomeza vitisho vya nyuklia.
Msaidizi wa Katibu Mkuu wa Umoja wa Mataifa, Khaled Khiari ametoa wito huo wakati akihutubia Baraza juu ya hatua za Umoja wa Mataifa kufuatia tukio hilo, sambamba na hofu yake kwa hali ya kibinadamu nchini DPRK, ambayo hujulikana pia kama Korea Kaskazini.
Kombora hilo la masafa marefu, lilirushwa kutoka jimbo la kaskazini la Jagang Oktoba 3, 2022 la Korea Kaskazini na likavuka eneo la ardhi la kilometa 4,500 na umbali angani wa kilometa 970, na mara ya mwisho kwa nchi hiyo kurusha kombora la masafa marefu kupita Japani, ilikuwa Septemba 15, 2017.
Hata hivyo, Katibu Mkuu wa UN, António Guterres aliisihi Korea Kaskazini kusitisha mara moja vitendo vya kuleta vurugu na kutoa wito kwa taifa hilo la barani Asia, kurejea katika mashauriano ili kuachana na uendelezaji wa nyuklia kwenye rasi ya Korea, na mwezi uliopita, shirika la Umoja wa Mataifa la nishati ya atomiki, IAEA, liliripoti kuwepo kwa viashiria vya majaribio ya nyuklia wa Punggye-ri.