Wataalamu wa haki za binadamu wa Umoja wa Mataifa, wanaohudumia watoto, wametoa taarifa ya pamoja wakisema majanga ya kiafya, kibinadamu na yale yanayohusiana na tabianchi yakizidi kuongeza changamoto duniani ikiwemo ukimbizi wa ndani, ukatili wa kingono na njaa.

Wataalamu hao, wameyasema hayo jijini Geneva, Uswisi na kuongeza kuwa Serikali lazima zikumbuke kuwa watoto wana haki kamilifu za kimsingi za kibinadamu na kwamba haki hizo zinapaswa kulindwa na kwamba mtu yeyote mwenye umri wa chini ya miaka 18 ni mtoto na anapaswa kupewa kipaumbele.

Taarifa nyingine iliyotolewa New York, Marekani pia imetaja wataalamu hao kuwa ni wale wa kamati ya Umoja wa Mataifa kuhusu haki za mtoto, Mwakilishi Maalum wa Katibu Mkuu wa Umoja wa Mataifa wa watoto kwenye mizozo ya kivita, Mwakilishi Maalum wa Katibu Mkuu wa UN wa ukatili dhidi ya watoto, UNICEF na ofisi ya Umoja wa Mataifa ya kukabili uhalifu na madawa ya kulevya.

Aidha, wamesema, mbali na nchi wanachama wa Umoja wa Mataifa lazima kutambua kuwa watu wote wenye umri wa chini ya miaka 18 ni watoto pia wanapaswa kuelewa kwamba Watoto wana haki mahsusi kwa mujibu wa Mkataba wa Kimataifa (CRC), ambazo ni kuishi, kuendelezwa, kulindwa na kushirikishwa.

“Tunasisitiza kuwa nchi wanachama zina wajibu wa kulinda, kuheshimu na kutekeleza haki za mtoto iwe wakati wa vita au wakati wa amani bila kujali umri, jinsia, hadhi, nchi anakoishi, au anakotoka, Watoto wote wanastahili kupatiwa haki zao ikiwemo ya kuishi, kuendeleza, kufurahia afya bora, akili, elimu, kucheza na kulindwa dhidi ya ukatili wa aina yoyote,” wamefafanua wataalamu hao.

Hata hivyo, wamesema hofu yao kubwa ni mazingira ambayo watoto wenye umri fulani kuchukuliwa kuwa ni watu wazima au kijana katika baadhi ya matukio, kwa kisingizio cha mila na utamaduni au harakati za kukabili ugaidi na hivyo kuwazuia haki yao ya msingi ya kufurahia haki zao kwa mujibu wa CRC.

Idadi wagonjwa wa afya ya akili yaogofya
Kituo magonjwa ya mlipuko kujengwa Kagera