Mawaziri wa mambo ya nje wa nchi za Misri na Ugiriki wamekutana mjini Cairo kwa maongezi kufuatia mikataba yenye utata ya bahari na gesi ambayo mpinzani wao wa pamoja Uturuki ilitia saini na kiongozi wa Libya.
Cairo na Athens, zimeimarisha uhusiano katika miaka ya hivi karibuni, ikiwa ni pamoja na ushirikiano katika kuendeleza rasilimali za nishati, kupambana na ugaidi na kutia saini mikataba mipya ya mpaka wa baharini na Cyprus.
Katika mkutano wa pamoja na waandishi wa habari, Waziri wa Mambo ya Nje wa Ugiriki, Nikos Dendias alisema mazungumzo na mwenzake wa Misri, Sameh Shukry yalilenga hati za maelewano kati ya Uturuki na Abdul Hamid Dbeibah, kiongozi wa mojawapo ya serikali mbili zinazoshindana katika Libya iliyogawanyika.
Amesema, mikataba hiyo ni tishio kwa utulivu wa kikanda iliyotiwa saini wiki iliyopita katika mji mkuu wa Libya, Tripoli ni pamoja na uchunguzi wa pamoja wa hifadhi za hydrocarbon katika maji ya pwani ya Libya na eneo la kitaifa ingawa Dendias alikashifu mikataba hiyo akisema ni haramu na ilikiuka sera za maji za Ugiriki.
Aidha, Waziri wa Mambo ya Nje wa Misri alisema Serikali ya Dbeibah haina mamlaka ya kuhitimisha mikataba hiyo, ikizingatiwa kwamba muda wake uliisha kufuatia kushindwa kwa Libya kufanya uchaguzi wa nchi nzima mwezi Desemba mwaka jana na kutoa wito kwa Umoja wa Mataifa kuchukua msimamo wa wazi juu ya uhalali wa serikali ya Dbeibah, akisema shirika la kimataifa halipaswi kunyamaza.
Makubaliano ya Uturuki na serikali ya Dbeibah yalikuja miaka mitatu baada ya makubaliano mengine yenye utata kati ya Ankara na serikali ya zamani ya Tripoli mwaka 2019, ukiipa Uturuki ufikiaji wa eneo linaloshindaniwa la Bahari ya Mediterania na kuchochea mvutano uliokuwepo awali wa Uturuki na Ugiriki na Kupro na Misri juu ya haki za uchimbaji visima katika eneo hilo.