Wapinzani wa Simba SC kwenye Michuano ya Ligi ya Mabingwa Barani Afrika Primero de Agosto wanatarajiwa kuwasili jijini Dar es salaam Ijumaa (Oktoba 14) wakitokea kwao Luanda-Angola, tayari kwa mchezo wa Mkondo wa Pili utakaopigwa Jumapili (Oktoba 16).
Simba SC itakua mwenyeji wa mchezo huo utakaounguruma Uwanja wa Benjamin Mkapa jijini Dar es salaam kuanzia saa kumi jioni, ikiwa mbele kwa ushindi mabao 3-1 uliopatikana ugenini Jumapili (Oktoba 09).
Meneja wa Habari na Mawasiliano wa Simba SC Ahmed Ally amezungumza na Waandishi wa Habari leo Jumatano (Oktoba 12) mchana na kuthibitisha ujio wa Primero de Agosto, ambayo ina Mlima mrefu wa kupanda kutokana na matokeo waliyoyavuna nyumbani.
Ahmed amesema Msafara wa de Agosto utawasili Dar es salaam majira ya mchana siku ya Ijumaa, huku akitoa rai kwa mashabiki ambao watapenda kuwapokea kufanya hivyo bila kuhofia chochote.
“Wageni wetu Primeiro de Agosto watawasili nchini Oktoba 14 majira ya mchana, kwa wale ambao wangependa kwenda kuwapokea wanakaribishwa uwanja wa ndege. Waamuzi wanatokea Afrika Kusini na watawasili nchini siku hiyo hiyo ya Oktoba 14.” amesema Ahmed Ally
Katika hatau nyingine Ahmed Ally amesema bado Simba SC haijafuzu hatua ya Makundi Ligi ya Mabingwa Barani Afrika licha ya kuongoza kwa mabao 3-1 dhidi ya Primero de Agosto ya Angola.
“Tulishinda lakini bado hatujafuzu, safari hii hatutaki kurudia makosa. Tumeweka nguvu kubwa kuona kwamba mchezo wa jumapili tunapata matokeo mazuri ili tuingie makundi. Tumemiss kushiriki hatua ya makundi ya Ligi ya Mabingwa Afrika.”
Msimu uliopita Simba SC ilipoteza nafasi ya kucheza Hatua ya Makundi Ligi ya Mabingwa kwa kupoteza nyumbani 3-1 dhidi ya Jwaneng Galaxy ya Botswana, ambayo ilikubaki kufungwa mjini Gaberone kwa mabao 2-0.
Mchezo wa Jumapili (Oktoba 16) dhidi ya Primero de Agosto Simba SC itahitaji ushindi ama sare yoyote katika ili kujihakikishia nafasi ya moja kwa moja kucheza Hatua ya Makundi Ligi ya Mabingwa Barani Afrika.