Ofisi ya Wakili Mkuu wa Serikali (OWMS), imeendelea kuiwakilisha Serikali katika usimamizi wa mashauri ya madai na usuluhishi, na kufanikiwa kuendesha mashauri ya madai na usuluhishi 6,043 kwa kipindi cha miaka minne tangu kuanzishwa kwake 2018.

Naibu Wakili Mkuu wa Serikali, Dkt. Boniphace Luhende ameyasema hayo, wakati akizindua Baraza la kwanza la wafanyakazi wa OWMS jijini Dodoma na kusema wameendesha mashauri hayo kwa niaba ya Serikali, ili kuendelea kutekeleza majukumu ya OWMS, ili kufikia na hata kuzidi matarajio ya Serikali.

Amesema OWMS imeendelea kuiwakilisha Serikali Mahakamani na katika mabaraza ya usuluhishi ambapo tangu kuanzishwa kwake imeendesha mashauri ya madai yapatayo 5,885 na mashauri ya usuluhishi 158 na kufanya jumla ya mashauri kuwa 6,043.

“Mashauri ya Madai yaliyomalizika katika kipindi cha miaka minne ni mashauri 582 na ya Usuluhishi ni mashauri 60 ambapo kati ya hayo, Serikali imeshinda mashauri 530 ya madai na Mashauri ya Usuluhishi 31”, ameongeza Dkt. Luhende

Awali, Wakili wa Serikali Mwandamizi, Bi Jenipher Kaaya ambaye pia ni mjumbe wa Baraza hilo amesema kuwa OWMS inafanikiwa kumaliza mashauri nje ya mahakama au mabaraza ya usuluhishi kwa kufanya majadiliano na wale wanaoidai Serikali kwa kuweka masuala ya kisheria pembeni na kujadili hoja kama watu wa kawaida na hatimaye kufika mwafaka na kuweza kushinda mashauri hayo.

Mkurugenzi wa Utawala na Utumishi wa OWMS, James Kibamba ametoa rai kwa wajumbe hao kuhakikisha kuwa masuala wanawakilisha vema watumishi wengine na kuwapatia mrejesho kwa kuwa sio rahisi kwa watumishi wote kuwa wajumbe wa Baraza.

Wizara yatadhaharisha matumizi, wizi wa mtandao
KMC FC yaapa kuifunga Mtibwa Sugar Uhuru Stadium