Balozi wa Uholanzi nchini Tanzania, Wiebe De Boer amewataka waandishi wa habari kushirikiana na wadau kuhamasisha mazingira wezeshi ya uhuru wa habari hapa nchini.

Balozi De Boer, ametoa wito huo jijini Dar es Salaam wakati akifungua warsha maalumu iliyoandaliwa na Jukwaa la Wahariri Tanzania (TEF) kwa wajili ya kuwajengea uwezo wahariri na waandishi wa habari kuhusu mabadiliko ya Sheria ya Huduma za Habari.

Amesema, uhuru wa vyombo vya habari ni muhimu kwa maendeleo ya taifa kwa sababu inaongeza uwazi na uzalishaji katika maeneo ya kazi na kwamba endapo vitakuwa huru, vinaweza kuwa mhimili wa nne wa utawala.

Balozi wa Uholanzi nchini Tanzania Dkt. Wiebe de Boer (katikati), akiwa na Mwenyekiti wa Jukwaa la Wahariri Tanzania (TEF), Deodatus balile (kushoto), na Mkurugenzi Mtendaji wa Kampuni ya Mwananchi Communication, ambaye pia ni Makamu Mwenyekiti wa TEF Bakari Machumu (kulia).

“Nafurahi kuona idadi nzuri ya wanawake katika majadiliano haya ya kuhusu Sheria za Habari, hili ni muhimu pia ninatarajia wataongezeka zaidi katika kuhamasisha mazingira wezeshi ya uhuru wa habari,” alisema Balozi De Boer.

Awali, Mwenyekiti wa Jukwaa la Wahariri nchini (TEF), Deodatus Balile alisema “Kuna mafanikio mengi sana katika kampeni ya kuhamasisha mabadiliko ya sheria hii, nikitaja yapo zaidi ya 20. Hii inatokana na msaada mnaotupatia.”

Balile ameongeza kuwa, mwamko wa uhamasishaji wa mabadiliko ya Sheria ya Huduma za Habari umeongezeka na kuleta matokeo chanya ikiwemo kufunguliwa kwa magazeti ya Tanzania Daima, Mseto, Mawio na MwanaHalisi.

Malaria bado 'kaa la moto' nchini
Habari Kuu kwenye magazeti ya leo Octoba 21, 2022