Mjumbe wa Kamati Tendaji ya Jukwaa la Wahariri Tanzania (TEF), Salim Said Salim amewataka waandishi wa habari hapa nchini wametakiwa kusoma sheria zinazohusu masuala ya habari na nyingine ili wanapotaka zirekebishwe wawe na ushawishi mkubwa kwa watunga sheria na jamii.

Ameyasema hayo wakati akifungua warsha ya kuwajengea uwezo wahariri juu ya mipango ya uchechemuzi wa mabdiliko ya sheria za habari.

Salim amesema kuwa mwandishi wa habari akijua haki zake, sheria zinazoongoza tasnia ya habari ataweza kukutana na makundi mbalimbali ya jamii ikiwemo wabunge na kuwashawishi juu ya sheria zinaminya uhuru wa habari na haki za binadamu.

“Bado waandishi hatujawa na uelewa mpana wa sheria zinazotuhusu, tufanye jitihada kuzijua. Tuwashawishi wenzetu juu ya sheria zinazokwaza ukuaji wa tasnia ya habari na maendeleo ya Taifa” amesema Salim.

Naye Mwenyekiti wa TEF, Deodatus Balile, amesema wataendelea kuwa mstari wa mbele kupigania mabadiliko ya sheria zinazogusa tasnia ya habari kwa kushirikiana na wadau wengine.

“Tunajipanga kuhakikisha tunakuwa sehemu ya kutatua matatizo yetu na yanayotukabili jamii, hatuwezi kutaka marekebisho ya sheria pasi na kushirikiana na Serikali kwa kushirikiana na wadau mbalimbali” amesema.

Naye mwezeshaji Tumaini Mbibo, amesema ni muhimu kwa waandishi wa habari kujua kiini cha matatizo yanayolikabili Taifa na njia za kutumia ili kutafuta ufumbuzi wa matatizo husika.

Amesema haki za binadamu zinakwenda sambamba na demokrasia hivyo uwepo wa sheria zinazominya tasnia ya habari zinakwamisha maendeleo hivyo vema ikafanyika mipango ya kufanya ushawishi wa mabadiliko.

Sylvester Hanga amesema waandishi wa habari wanataka sheria za masuala ya habari ziwe rafiki ili zichochee demokrasia, haki za binadamu na maendeleo kwa Taifa.

“Waandishi wa habari ni lazima wawe mstari wa mbele kuisemea jamii lakini ni lazima wahakikishe sheria zinazominya uhuru wa habari zinafanyiwa marekebisho kwa kushirikiana na wadau mbalimbali” amesema.

Balozi wa Uingereza awapa Polisi mbinu
Moto wazuka mlima Kilimanjaro