Matokeo ya Sensa ya Watu na Makazi iliyofanyika mwezi Agosti, 2022 yametangwazwa na kuonesha kuwa idadi ya watanzania imefikia watu milioni 61,741,120, ambapo wanawake wapo milioni 31.6 sawa na asilimia 51 huku Wanaume wakiwa ni milioni 30.5 sawa na asilimia 49.
Takwimu hizo, zimetangazwa na Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Samia Suluhu Hassan hii leo (Jumatatu Oktoba 31, 2022), katika Uwanja wa Jamhuri jijini Dodoma, na kusema kati ya watu hao milioni 61.74, Watu milioni 59.8 wako Tanzania Bara, na Watu milioni 1.8 wako Zanzibar.
Amesema, “Niseme nisiseme, Napenda kuwatanzangia kuwa Tanzania ina idadi ya watu milioni 61.74. kati yao wanawake ni milioni 31.6 sawa na asilimia 51 na wanaume milioni 30.53 sawa na asilimia 49 ya watu wote.”
Rais Samia ameongeza kuwa, Mkoa wa Dar es Salaam ndio unaongoza kwa kuwa na idadi kubwa ya watu nchini, wanaofikia milioni 5.3 sawa na asilimia 7, ukifuatiwa na Mkoa wa Mwanza wenye watu milioni 3.6 sawa na asilimia 6 ambapo katika kipindi cha miaka 10 lipo ongezeko la watu milioni 16.8 ambalo ni sawa na asilimia 3.2.
“Miaka kumi iliyopita Tanzania ilikuwa na watu 44, 928, 923 hii inaonyesha kumekuwapi na ongezeko la watu milioni 16,812,197 sawa na ongezeko la asilimia 3.2 ya waliokuwepo kati ya mwaka 2012 na mwaka 2022 na Tanzania Zanzibar, idadi ya watu imeongezeka kutoka 1,303,569 mwaka 2012 hadi watu 1, 889,773 mwaka 2022 sawa na ongezeko la asilimia 3.7” amebainisha Rais Samia.
Sensa ya watu na makazi, hufanyika kila baada ya miaka 10, ambapo sensa ya mwaka 2022 ni ya sita kufanyika nchini baada ya Muungano wa Tanganyika na Zanzibar mwaka 1964 na zingine zilifanyika mwaka 1967, 1978, 1988, 2002 na 2012 huku matokeo ya mwaka 2012 yakionesha Tanzania kuwa na watu 44,929,002 ambapo 43,625,434 ni wa Tanzania Bara na 1,303,568 wa Zanzibar.