Kamisaa wa Sensa, Anne Makinda amesema umati mkubwa ya watu waliojitokeza katika utoaji wa matokeo ya Sensa ya watu na makazi ya mwaka 2022 hii leo Oktoba 31, 2022 ni uthibitisho tosha kuwa zoezi hilo lilipokelewa kwa shauku na Wananchi ambao kwa pamoja wamefanikisha kufikia tamati ya hitaji hilo.

Makinda ameyasema hayo jijini Dodoma, katika zoezi la utoaji wa Matokeo ya Sensa na Watu na Makazi ya Mwaka 2022 linalofanyika katika Uwanja wa Jamhuri na kuongeza yatasaidia kujua namna ambavyo serikali itawahudumia wananchi wake kwa ufanisi baada ya kujua idadi yao kamili katika sehemu hii ya kwanza kwa mujibu wa kalenda.

Amesema, “Wakati tunawahamasiasha wananchi kushiriki zoezi hili la sensa tuliwaelekeza wananchi namna ambavyo litatusaidia kujua mustakabali wa maenedeleo yetu maana ili kuweza kuwahudumia watu ni muhimu kujua idadi yao na hii itasaidia katika kupanga utoaji wa huduma kwa uhakika.”

Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Samia Suluhu Hassan (katikati), akiwa na Rais wa Zanzibar na Mwenyekiti wa Baraza la Mapinduzi, Dkt. Hussein Ally Mwinyi (kushoto), na Waziri Mkuu, Kassim Majaliwa (kulia), kwenye uwanja wa Jamhuri jijini Dodoma wakati wa zoezi la utangazaji wa matokeo ya Sensa ya watu na makazi, hii leo Oktoba 31, 2022.

Sensa ya watu na makazi itaisaidia Serikali kupata taarifa za msingi zitakazosaidia mchakato wa utekelezaji wa Dira ya Maendeleo ya mwaka 2025, mageuzi ya masuala ya afya na jamii, pamoja na ufuatiliaji wa ajenda za maendeleo za kimataifa na utekelezaji wa mipango ya maendeleo ambayo huakisi matakwa ya watu katika ngazi husika na kwenye uwiano wa mgawanyo wa rasilimali.

Umuhimu mwingine ni pamoja na kupata taarifa za msingi za hali ya kidemografia, kijamii na kiuchumi za idadi ya watu na makazi za mipango katika ngazi zote, na kigawio katika kukokotoa viashiria vingine vya pato la mtu mmoja mmoja, Taifa, Ajira na ukosefu wa Ajira na kiwango cha uandikishaji wa wanafunzi.

Aidha, taarifa hizo pia zitasaidia kuiwezesha serikali kujua ongezeko la idadi ya watu, kwa mgawanyo na viashiria vingine, ambavyo ni muhimu kwa usimamizi wa mazingira na msingi wa utawala bora na ujumuishaji wa demokrasia, na ugawaji wa majimbo ya uchaguzi kwa ufanisi na kurekebisha mipaka ya kiutawala katika serikali za mitaa.

Waandamana kupinga upatanishi wa raia na Jeshi
Kocha Mtibwa Sugar ataja sababu za kipigo cha 5-0