Bunge la Kenya, limeidhinisha upelekaji wa kikosi kipya cha Wanajeshi 1,000 eneo la mashariki mwa Jamhuri ya Kidemokrasia ya Kongo DRC, huku kukiwa na maswali kuhusu gharama ya dola milioni 37 kwa miezi sita ya kwanza Kikosi hicho.
Ripoti ya kamati ya bunge la nchi hiyo, inasema fedha hizo zitatumika kununua vifaa, posho na operesheni kwa zaidi ya wanajeshi 900 wanaojiunga na Kikosi cha Kanda ya Jumuiya ya Afrika Mashariki, kitakachosaidia vikosi vya Kongo dhidi ya makundi yenye silaha.
Hata hivyo, Wabunge wa upinzani walihoji ni kwa nini Kenya inatumia pesa nyingi kwa misheni ya kanda, huku nchi hiyo ikikabiliwa na masuala yake ya usalama na ongezeko la mfumuko wa bei na deni kubwa la umma.
Mapema hivi karibuni, Rais wa Kenya, William Ruto aliitaja misheni hiyo kuwa ni ya lazima na ya dharura kwa usalama wa kikanda huku Ghasia zinazofanywa na makundi yenye silaha mashariki mwa Kongo zikisababisha mzozo wa kidiplomasia kati ya Kongo na nchi jirani ya Rwanda.