Katika kukabiliana na changamoto ya upungufu wa maji katika maeneo mbalimbali nchini Wizara ya maji imejipanga kuchimba mabwawa kwa ajili ya uvunaji wa maji ya mvua na kuyaingiza katika mfumo.

Hayo yamebainishwa hii leo Novemba 10, 2022 na Waziri wa Maji, Jumaa Aweso ambaye pia ametumia fursa hiyo kumshukuru Rais Mheshimiwa Samia Suluhu Hassan kwa kuwawezesha kupata mitambo ya kuchimba visima ili kukabiliana na upungufu wa maji.

Amesema, mahitaji ya maji katika mkoa wa Dar Es Salaam ni lita milioni 544 kwa siku na uzalishaji maji kwa siku ni lita milioni 520 katika kipindi ambacho kiwango cha maji katika Mto Ruvu kinakuwa katika hali ya kawaida, hivyo kuwa na upungufu wa lita zaidi ya milioni 24.

Waziri Aweso ameongeza kuwa, “Katika kipindi hiki ambacho kiwango cha maji kimepungua katika Mto Ruvu uzalishaji wa maji nao umepungua na kufikia lita milioni 300 kwa siku, hivyo kusababisha upungufu wa lita milioni 244.”

Amesema, “Baada ya kuingiza lita milioni 70 kutoka katika mradi wa visima vya Kigamboni na lita milioni 29.4 kutoka katika mradi wa visima vingine 160 vya jijini Dar es Salaam, upungufu wa maji ni lita milioni 145 kwa siku, hivyo kupunguza changamoto ya upatikanaji wa maji katika baadhi ya maeneo jijini humo.”

Serikali yataka tathimini ya haraka kubomoka kwa Bwawa la tope
Mtaturu aibana Serikali ujenzi Kituo cha Polisi