Mshambuliaji wa Klabu ya RB Leipzig ya Ujerumani Christopher Nkunku atazikosa Fainali za Kombe la Dunia zitakazoanza kurindima mwishoni mwa juma hili (Novemba 20) nchini QATAR.

Mshambuliaji huyo mwenye umri a miaka 25, amepatwa na majeraha ya mguu akiwa katika mazoezi ya mwisho ya kikosi cha Ufaransa kabla ya kuanza safari ya kuelekea nchini QATAR.

Nkunku alipatwa na majeraha hayo baada ya kugongana na Kiungo wa klabu ya Real Madrid Eduardo Camavinga.

Nkunku anaungana na wachezaji wengine wa Ufaransa ambao walipewa nafasi kubwa ya kuitwa na Kocha Didier Claude Deschamps, lakini aliwatema kutokana na sababu za kuwa majeruhi.

Wachezaji hao ni Viungo Paul Pogba, N’Golo Kante pamoja na Beki Prisnel Kimpembe.

Hata hivyo bado Kocha Deschamps, bado hajatangaza mbadala wa Nkunku hadi sasa.

Ufaransa inatarajiwa kuanza safari ya kuelekea QATAR leo Jumatano (Novemba 16) tayari kwa Fainali za Kombe la Dunia, huku ikipangwa Kundi D sambamba na timu za mataifa ya Tunisia, Australia na Denmark.

Ufaransa itaanza kampeni ya kutetea Ubingwa wa Dunia Novemba 22 kwa kucheza dhidi ya Australia katika Uwanja wa Al Janoub, uliopo mjini Al Wakrah.

Mchezo wa pili Ufaransa itacheza dhidi ya Denmark Novemba 26 mjini Doha katika Uwanja wa 974 na itamaliza Michezo ya Hatua ya Makundi kwa kupapatuana na Tunisia Novemba 30 mjini Al Rayyan kwenye Uwanja wa Education City.

Haaland kucheza Ligi Daraja la 7 England
Infantino aomba mzozo wa Urusi, Ukraine usitishwe