Mwenyekiti wa Klabu ya Simba SC Murtaza Mangungu amewataka wadau wa Soka nchini Kuheshimu na Kuamini ufafanuzi uliotolewa na Klabu hiyo kuhusu Kocha wa Makipa Muharami Said Mohammed maarufu ‘Shilton’.

Simba SC ilitoa taarifa za kutomtambua Kocha huyo kama Mwajiriwa wake, baada ya kutoka kwa taarifa za kutuhumiwa na dawa za kulevya iliyotolewa jana Jumanne (Novemba 15), Kamishna Jenerali wa Mamlaka ya Kudhibiti na Kupambana na Dawa za Kulevya Tanzania (DCEA) Gerald Kusaya katika Mkutano na Waandishi wa Habari.

Mangungu amesema Kocha Muharami alichukuliwa Simba kwa makubaliano ya muda mfupi na hakuajiriwa kama Kocha wa Makipa wakati wote alipokua kwenye Benchi la Ufundi msimu huu 2022/23.

“Watu watulie, kocha Muharami alikuwa kwa muda Simba. Alikuwa kwenye benchi letu kwa mechi kadhaa, ikiwamo ya Malawi (Big Bullets) na kwenye mechi na Angola, lakini yule ni Kocha wa Cambiasso, kilichotokea ni masuala yake binafsi.” amesema Mangungu

Tayari Simba SC imemtangaza Kocha wa Makipa Zakaria Chlouha raia wa Morocco Kuwa Kocha Mpya wa Walinda Lango.

Kabla ya kutua Simba, Zakaria Chlouha mwenye umri wa miaka 48 alikuwa akiifundisha Klabu ya Al Urooba kutoka Falme za Kiarabu (U.A.E).

Eddy Kenzo atajwa tuzo za Grammy 2023
Polisi yaanza uchunguzi vifo vya wawili