Kocha Mkuu wa Ihefu FC Juma Mwambusi amesema yupo tayari kwa lolote kuelekea mchezo ujao wa Ligi Kuu Tanzania Bara dhidi ya Mabingwa Watetezi Young Africans.
Miamba hiyo ya Ligi Kuu itakutana kesho Jumanne (Novemba 29) katika Uwanja wa Kumbukumbu ya Sokione jijini Mbeya, kuanzia mishale ya saa kumi jioni.
Kocha Mwambusi amesema baada ya kupoteza michezo kadhaa, atahakikisha kikosi chake kinakwenda kupambana kwa lengo la kupata matokeo pasina kuihofia Young Africans, ambayo itakua ikisaka rekodi ya kucheza michezo 50 bila kufungwa.
Amesema anaifahamu vizuri Young Africans huku akieleza wapinzani wao wamekua na msimu mzuri tangu mwanzo, hivyo watacheza kwa kuwaheshimu pasi na kupoteza lengo lao la kusaka alama tatu ambazo zitawasidia katika hesabu siku zao siku za usoni.
“Litakalokuwa na liwe, dakika 90 ndio zitaamua, tunawaheshimu wapinzani wetu kwa kuwa wamekuwa na msimu mzuri, ila tutapambana nao kadri ya uwezo wetu kusaka alama tatu,” amesema Mwambusi
Ihefu FC inakwenda kukutana na Young Africans ikiwa katika nafasi ya mwisho katika msimamo wa Ligi Kuu, ikifikisha alama 08, wakicheza michezo 13.