Mashabiki wa Soka wa Qatar, wametumia picha za mchezaji mkubwa wa Ujerumani aliyestaafu kuichezea timu ya taifa, Mesut Ozil kuwakashifu wachezaji na mashabiki wa timu hiyo, ikiwa ni hatua ya kulipa kisasi.

Tukio hilo limetokea kwenye mchezo wa Kombe la Dunia kati ya Ujerumani na Hispania uliopigwa jana Jumapili (Novemba 27)na kumalizika kwa sare ya 1-1, ambapo mamia ya mashabiki wa Qatar walionekana wakiwa wamebeba picha ya mchezaji huyo, ambaye alilazimika kustaafu kuichezea timu ya taifa kutokana na madai ya ubaguzi wa rangi.

Kitendo hicho kimetafsiriwa kama ni hatua ya mashabiki wa Qatar kulipa kisasi, kufuatia wachezaji wa Ujerumani kupiga picha katika mchezo wao wa kwanza, wakiwa wamejiziba midomo yao.

Kitendo hicho kilitafsiriwa kama ishara ya kuonesha kugomea uamuzi wa Qatar kupiga marufuku manahodha wa timu za Ulaya, kuvaa vitambaa vya One Love mikononi mwao, vinavyotajwa kuwa ni ishara ya kuunga mkono mapenzi ya jinsia moja.

Hoja iliyojengwa na Ujerumani, ilikuwa ni kutaka kuifanya Dunia ilione taifa la Qatar kama nchi inayokandamiza haki za binadamu na kuleta ubaguzi.

Hata hivyo, ni kama kibao kimewageukia kutokana na kuwepo kwa kumbukumbu mbaya ya mchezaji wa Ujerumani, Mesut Ozil kubaguliwa na kunyanyaswa kwa sababu ya asili yake kuwa ni Uturuki, kiasi cha kulazimika kustaafu kuitumikia timu hiyo ya taifa.

Mayele atangaza njaa ya mabao Ligi Kuu
Mwambusi: Dakika 90 zitaamua, Liwano na liwe