Polisi nchini Zambia wamesema wamepata miili ya watu 27, wanaoaminika kuwa wahamiaji kutoka Ethiopia, ikiwa imetupwa kwenye eneo moja la shambani kwenye viunga vya mji mkuu wa Lusaka wakihisiwa kufariki kutokana na uchovu.
Katika tukip hilo, manusura mmoja alipatikana na kukimbizwa hospitali ya Lusaka kwa ajili ya kupewa matibabu, wakati waliokufa walisafirishwa hadi chumba cha kuhifadhi maiti ambako watafanyiwa uchunguzi na kutambua kilichosababisha vifo vyao.
Uchunguzi wa awali wa Polisi, unaonyesha kuwa wahanga hao ambao wote ni wanaume wa umri wa kati ya miaka 20 na 38 walitupwa kando ya barabara na watu wasiojulikana.
Msemaji wa Polisi, Danny Mwale amesema polisi na maafisa wengine wameanzisha uchunguzi ili kuweza kubaini uhalisia wa tukio hilo na kuchukua hatua stahiki.