Tanzania imetajwa kuwa katika hali mbaya ya kimazingira na kwamba endapo Serikali haitachukua hatua za haraka basi maafa makubwa yatazidi kujitokeza katika jamii kutokana na uharibifu wa misitu na vyanzo vya maji katika maeneo mengi ikiwemo bonde la mto Ruaha.
Hayo amesema na Mwenyekiti wa kituo cha Wanahabari watetezi wa rasilimali na taarifa (MECIRA), Habibu Mchange wakati akiongea mbele ya mgeni rasmi wa Kongamano la Wahariri na Wadau wa Uhifadhi, Mazingira na utunzaji wa vyanzo vya maji, Makamu wa Rais wa Tanzania, Philip Mpango.
Amesema, “Mheshimiwa Makamu wa Rais hali ni mbaya ni siku ya 130 leo mto Ruaha hautiririshi maji, wanyama wanakufa, mito inakauka, watu wanachepusha maji na wasaidizi wenu wapo, inasikitisha sana watu wachache waharibifu hawawezi kuwaumiza wananchi wasio wengi pambaneni katika hili inawezekana.”
Mchange ameongeza kuwa, “Ukitembea au ukipita angani ukaona uharibifu huo utaumia na kibaya ni kaya chache tu zinafanya haya lakini athari zake zinawakumba wengi, leo mtu anasimama kupambania aendelee kuchepusha maji au kulima kando kando ya mto jeuri hii anaitoa wapi.”
Naye Mwenyekiti wa Jukwaa la Wahariri nchini TEF, Deodatus Balile akiongea katika Kongamano hilo amesema inasikitisha kuona uharibifu ukiendelea na wenye mamlaka wapo kimya wakati uwezo wa kusimamia na kuthibiti hali hiyo wanao.
Amesema, “Unakuta mtu anachunga Ng’ombe kwenye hifadhi na akikamatwa cha ajabu anayepiga simu ziachiwe anakuwa Naibu Waziri, hii haijakaa sawa na tukisema tunakuwa hatarini lakini sasa inatubidi inatubidi tuseme maana hali ni mbaya.
Hata hivyo, wameishauri Serikali kuchukua hatua za ziada kwa kuwawajibisha watendaji wake wasio waaminifu, ambao wamekuwa wakishirikiana na majangili wa uhifadhi ili kuokoa hali mbaya inayoendelea kuitafuna nchi na kusababisha madhara kwa jamii, mimea na wanyama.