Kaimu Kocha Mkuu wa Simba SC Juma Ramadhan Mgunda amesema anaiheshimu Timu ya Kagera Sugar inayonolewa na Kocha Mecky Mexime, ambayo kesho itakua nyumbani UWanja wa Kaitaba ikiwania alama tatu dhidi ya Mnyama.

Simba SC itacheza ugenini katika mchezo wa pili wa Mzunguuko wa Pili wa Ligi Kuu Tanzania Bara, ikitangulia kufanya hivyo dhidi ya Geita Gold FC juzi Jumapili (Desemba 18), na kuibuka na ushindi wa 5-0 katika Uwanja wa CCM Kirumba.

Mgunda amekiri kuiheshimu Kagera Sugar alipozungumza na Waandishi wa Habari mjini Bukoba leo Jumanne (Desemba 20) majira ya Mchana katika Mkutano maalum kuhusu mchezo huo wa Ligi Kuu Tanzania Bara msimu huu 2022/23.

“Tunamshukuru Mungu tumewasili salama mjini Bukoba kwa ajili ya mchezo wetu wa kesho, nina uhakika utakua mchezo mgumu na mzuri, lakini tumejiandaa kupambana ili kupata matokeo mazuri.”

“Mecky Mexime ni Mdogo wangu lakini nimesoma naye Darasa moja, hilo linatosha kusema ninamuheshimu sana, hata timu yake ya Kagera Sugar ninaiheshimu sana, kwa sababu inacheza soka la ushindani, kwa hiyo kesho tutaingia Uwanjani tukitambua tunakwenda kucheza na timu ngumu.”

“Jambo la msingi tunapaswa kuwaombea wachezaji wa pande zote mbili waamke salama kesho ili kutupa burudani ya Soka, ninaamini wapo wanaopenda Soka na sio Mashabiki, hawa wanapaswa kupewa haki yao.” amesema Mgunda

Simba SC inakwenda katika mchezo huo huku ikiwa na kumbukumbu ya kufikisha alama 37 katika msimamo wa Ligi Kuu Tanzania Bara baada ya kuifunga Geita Gold FC, huku ikitanguliwa na Young Africans iliyo kileleni kwa kufikisha alama 41.

Ibrahim Ajib aondoka Azam FC
Taifa lina hali mbaya uharibifu wa mazingira: Mchange