Wachezaji Evarist Myauki na Ramadhani wapo mbioni kutimka Ihefu FC, kutokana na ofa iliyowekwa mezani huku baadhi ya timu zikiwataka kwa mkopo.
Dirisha Dogo la Usajili kwa Timu za Ligi Kuu Bara, Championship na First League, lipo wazi tangu Desemba 16, mwaka huu na linatarajiwa kufungwa Januari 15, mwakani, ambapo timu za ligi hizo zina nafasi ya kufanya maboresho katika vikosi vyao.
Kocha Mkuu wa Ihefu FC, Juma Mwambusi, amesema kuna ofa imeshuka klabuni hapo ya wachezaji wao kutakiwa na timu nyingine huku akiahidi kukifanyia maboresho kikosi chake baada ya kupungua wachezaji.
“Wachezaji wangu Evarist na Ramadhani wamepata ofa kuna timu zimejitokeza zikitaka kuwachukua katika Dirisha hili Dogo linaloendelea, bado tunaendelea na mazungumzo na timu husika mpango ukikamilika ndipo tutakapoziweka wazi timu hizo.”
“Pia, nahitaji kuongeza nguvu katika kikosi changu kwa kusajili wachezaji eneo la kati na ushambuliaji sehemu ambayo ndiyo nimepaangalia na kutakiwa maboresho.”
“Dirisha Dogo mara nyingi ni gumu kuweza kupata wachezaji kwa kuwa wengi hawapo huru wana mikataba yao, hivyo ni ngumu kumpata mchezaji yule unayemhitaji.”
“Wachezaji wanaopatikana sasa hivi ni kwa ugumu sana, hivyo tunafanya maboresho kulingana na wachezaji tutakaowapata,” amesema Mwambusi