Mabingwa wa Soka Tanzania Bara Young Africans wametangaza vita ya kisasi dhidi ya Ihefu FC, kuelekea mchezo wa Jumatatu (Januari 16).
Mchezo huo wa Mzunguuko wa 20 wa Ligi Kuu Tanzania Bara utashuhudia Young Africans ikicheza nyumbani Uwanja wa Benjamin Mkapa jijini Dar es salaam, huku ikikumbuka namna ilivyoadhiriwa ugenini Highland Estate pale Mbarali mkoani Mbeya kwa kuvunjiwa Rekodi yake ya kutokufungwa michezo 49 mfululizo.
Afisa Habari wa Young Africans Ally Kamwe amesema wamedhamiria kushinda Mchezo huo, sambamba na kulipa kisasi kwa Ihefu FC, ambayo wanatambua ina kikosi kizuri.
Amesema Idara zote Klabuni hapo zimejipanga kuhakikisha ushindi unapatikana Jumatatu (Januari 16), na ndio maana wachezaji wao wamerejea mazoezini wakiwa na ari kubwa.
“Ihefu FC itabidi watusamehe kwa kweli, kwa kuwa mchezo huu ambao tunakutana nao safari hii utakuwa ni mchezo wa kisasi, kwa kuwa tunafahamu ni kwa kiasi gani waliweza kutufunga wakiwa kwao, hivyo hatutakubali hili lijitokeze tena kwa mara nyingine.”
“Kuanzia Viongozi, Benchi la Ufundi hadi Wachezaji wote tunahitaji kuhakikisha kuwa tunapata ushindi, na Idara zote hizo tuna hasira na Ihefu FC, lazima tuhakikishe tunalipa kisasi dhidi yao.” amesema Ally Kamwe
Young Africans bado inaongoza msimamo wa Ligi Kuu Tanzania Bara ikifikisha alama 50, ikifuatiwa na Simba SC yenye alama 46, huku Ihefu FC ikiwa nafasi ya 13, ikimiliki alama 20.