Klabu ya Dodoma Jiji FC imefunguka usajili wa Mshambuliaji kutoka nchini Ghana Steven Sey, ambaye mwanzoni mwa juma hili alikamilisha taratibu za kujiunga na Klabu hiyo ya mjini Dodoma.

Afisa Habari wa Dodoma Jiji FC Moses Mpunga amesema, haikuwa rahisi kuipata saini ya Mshambuliaji huyo, ambaye amewahi kuzitumikia klabu za Singida united na baadae Namungo FC kabla ya kutimkia nchini Misri.

Mpunga amesema, Sey alikuwa ajiunge na Klabu yao mwanzoni mwa msimu huu, lakini ilishindikana kutokana na Dili lake kuingiliwa na Klabu Kongwe za Tanzania ambazo zina uwezo wa kifedha.

“Tumefanikiwa kumsajili Sey Mshambuliaji mwenye ubora na viwango vya hali ya juu, lakini pia ana uzoefu mkubwa wa Ligi yetu hapa nchini.”

“Sey alikuwa mmoja wa wachezaji ambao walipendekezwa na aliyekuwa Kocha Mkuu Masoud Juma mwanzoni mwa msimu huu, lakini ilishindikana kufuatia timu kubwa za Ligi Kuu kuingiza mkono kwenye usajili wake.”

“Ninaamini kuwa Sey atakuwa na mchango mkubwa sana kwenye kikosi chetu katika kipindi hiki cha Duru la Pili la Ligi Kuu, kwa sababu tunafahamu ana uzoefu mkubwa katika safu ya Ushambuliaji ambao utatuwezesha kufikia malengo yetu.” amesema Mpunga

Tahadhari yatolewa mlipuko wa kipindupindu
Simba SC, Makusu mambo yamenyooka