Wakala wa mshambuliaji kutoka DR Congo Jean Makusu Mundele amefunguka kwa undani Dili la mchezaji wake kukaribia kucheza katika Ligi Kuu Tanzania Bara msimu huu 2022/23.

Makusu ambaye kwa sasa yupo kwenye kikosi cha DR Congo kitakachoshiriki Fainali za Mataifa Bingwa Barani Afrika ‘CHAN’ nchini Algeria, anahusishwa na Klabu ya Simba SC inayosaka Mshambuliaji, baada ya Kocha Mkuu Robertinho kuuagiza Uongozi kufanya hivyo.

Faustino Mukandila, Wakala wa Mshambuliaji huyo amesema suala la Mchezaji wake kutua Tanzania na Kucheza Ligi Kuu ya Tanzania Bara linasubiri muda, lakini ana uhakika kila kitu kitakuwa wazi siku kadhaa zijazo.

Katika hatua nyingine Mukandila amekanusha taarifa za Makusu kuwindwa na Klabu ya Singida Big Stars, ambayo inashiriki kwa mara ya Kwanza Ligi Kuu Tanzania Bara msimu huu.

Amesema Mchezaji wake atacheza kwenye moja ya timu kubwa zinazowika katika Ligi hiyo, hivyo amewataka Mashabiki wa Soka kuendelea kuwa na subra.

“Mchezaji wangu atacheza moja ya timu kubwa hapo Tanzania, kwa sasa ni ngumu kulizungumza hilo lakini taarifa za mchezaji wangu kucheza Singida Big Stars hapana, hilo halipo katika mipango yetu kwa sasa.”

“Jambo ambalo ninataka kukuhakikishia kwa sasa ni kuhusiana na Makusu, ni lazima atacheza kwenye Ligi Kuu ya Tanzania Bara, hilo ninakupa kwa asilimia 100 kwa sababu ninajua nini ninamaanisha.” amesema Wakala huyo

Jean Makusu Mundele kwa sasa ni Mchezaji huru, baada ya kuvunja mkataba na Klabu ya FC Lupopo ya nchini kwao DR Congo, kufuatia tofauti zilizodumu kwa kipindi kirefu kati yake na Uongozi wa juu wa Klabu hiyo.

Dodoma jiji FC: Haikuwa rahisi kumsajili Sey
Wafanyabishara mashuhuri Afrika kuunda jukwaa