Msemaji Mkuu wa Serikali Gerson Msigwa amesema ndege mpya 5 zilizonunuliwa na serikali zinatarajiwa kuwasili nchini mwaka huu 2023, ili kuendelea kuimarisha zaidi Shirika la Ndege nchini (ATCL).
Ameyasema hayo wakati akizungumza na waandishi wa habari Jijini Dodoma, ambapo ameeleza kuwa kuwa Serikali ya Awamu ya Sita chini ya Rais Samia Suluhu Hassan, imedhamiria kuimarisha shirika hilo la ndege na kukuza utalii.
Msigwa amebainisha baadhi ya ndege hizo ambazo zitaanza kuwasili ni ndege ya mizigo aina ya Boeing 767-300, ambayo inatarajiwa kuingia nchini mwezi Machi na kufuatiwa na ndege mbili za abiria aina ya Boeing 737-9 Max, ambapo moja inatarajiwa kuingia nchini mwezi Julai na nyingine mwezi Oktoba.
Aidha, amesema ndege nyingine kubwa ya abiria aina Boeing 787-8 Dreamliner, ambayo inatarajiwa kuingia nchini mwezi Novemba.
Msigwa amesema kuwa serikali inaendelea na mazungumzo na watengenezaji wa ndege ya tano aina ya Bombardier Dash 8-Q400, ambayo ni ndege ya abiria, ili kujua itakuja linin a kuujulisha umma pindi watakapopata taarifa.