Mfungaji wa mabao ya Simba SC katika mchezo wa Kimataifa wa Kirafiki dhidi ya CSKA Moscow Habib Haji Kiyombo amemshukuru Kocha Mkuu Robertinho kwa kumpa nafasi ya kucheza mchezo huo.

Simba SC ilicheza mchezo wake wa pili na wa mwisho ikiwa kambini Dubai-Falme za Kiarabu dhidi ya CSKA Moscow jana Jumapili (Januari 15), na kuambulia matokeo ya sare ya 2-2, baada ya kupoteza 1-0 dhidi ya Dhafra FC ijumaa (Januari 13).

Kyombo amesema Kocha Robertinho ameonesha kumuamini na ndio maana alimpa nafasi ya kucheza katika mchezo huo, hivyo hana budi kushukuru kwa kupata nafasi hiyo.

Amesema anatambua Kocha huyo kutoka Brazil aliona umuhimu wake kumtumia kwenye mchezo huo, ambao amekiri kufurahia kwa kuisaidia timu yake ambayo ilikua nyuma kwa mabao 2-0, baada ya kipindi cha kwanza.

“Ninamshukuru Kocha kwa kuniamini nakunipa nafasi ya kucheza kwenye mchezo huu, ninaamini aliona kitu kutoka kwangu na aliponipa nafasi nilifuata maelekezo hadi kupata wasaa wa kuisaidia timu kwa kufunga mabao ya kusawazisha.”

“Kocha alituambia kila mmoja ana nafasi ya kucheza, kwangu ninashukuru kwa kunipa hiyo nafasi na nimeonesha uwezo, lakini bado ninasisitiza Simba sio mtu mmoja, Simba ni timu ya wachezaji wote.”

“Wakati ninaingia nilijua timu inahitaji msaada kutoka kwa wachezaji wote tuliokuwepo uwanjani, kufunga ni sehemu ya mchezo, lakini ninaamini ushirikiano wetu wote umetupa nafasi ya kumaliza tukiwa salama na kupata matokeo ya sare.” amesema Kyombo

Simba SC inatarajia kurejea nyumbani Tanzania, tayari kwa mchezo wa Mzunguuko wa 20 wa Ligi Kuu Tanzania Bara dhidi ya Mbeya City, utakaopigwa keshokutwa Jumatano (Januari 18), Uwanja wa Benjamin Mkapa jijini Dar es salaam.

Serikali yatoa ufafanuzi Airbus za ATCL
Emiliano Martinez awekwa kikaangoni FIFA