Mlinda Lango Metacha Mnata amewaomba radhi Mashabiki na Wanachama wa Klabu ya Young Africans, baada ya kusajiliwa kwa mkopo klabuni hapo.
Metacha amerudi Young Africans akitokea Singida Big Stars alikokuwa akicheza soka lake, baada ya kusajiliwa mwanzoni mwa msimu huu akitokea Polisi Tanzania.
Mlinda Lango huyo amelazimika kuomba radhi kufuatia utovu wa nidhamu alioufanya kabla ya kuondoka Young Afrika misimu miwili iliyopita.
Metacha ametoa kauli ya kuomba radhi dakika chache baada ya kukamilisha uhamisho wake usiku wa kuamkia leo akisema: “Ninayofuraha kubwa ya kuwajulisha nimepata nafasi ya kurudi tena kwenye klabu niipendayo ya Young Africans, nikiwa kama mpambanaji hapo nyuma lakini nilifanya makosa kwa hiyo ninaomba mnisamehe na mnipokee.”
“Ninaahidi kuwa Metacha wa sasa sio yule aliyekuwepo hapo nyuma, ninaahidi nitapambana kwa moyo mmoja na kwa ari kubwa, ili nihakikishe timu inapata matokeo, ninawaahidi nitafanya vizuri na nitakuwa bora zaidi.”
Metacha Mnata alionesha utovu wa nidhamu wakati wa mchezo wa Ligi Kuu msimu wa 2020/21 dhidi ya Ruvu Shooting, Baada kwa kuwaonesha ishara ya Kidole cha Kati Mashabiki wa Klabu ya Young Africans, ambao walimbeza kwa kiwango chake kwa siku hiyo.
Kufuatia kosa hilo, Kamati ya Saa 72 ilitangaza kumfungia Metacha, Michezo mitatu na kutozwa faini ya Shilingi Laki Tano.