Kama ulidhani Azam FC imekata tamaa ya Ubingwa wa Tanzania Bara msimu huu 2022/23 ulikuwa unakosea sana, kwani bado matumaini makubwa ya kuendelea kulisaka taji.
Azam FC inashika nafasi ya tatu katika msimamo wa Ligi Kuu Tanzania Bara ikiwa na alama 43, ikitanguliwa na Simba SC yenye alama 44 na Young Africans inaongoza ikiwa na alama 53.
Kocha Msaidizi wa Azam FC Aggrey Morrison amesema ni mapema mno kuiondoa Klabu yao katika mbio za ubingwa, kwani bado wanaamini nafasi hiyo wanayo na lolote linaweza kutokea.
Amesema mbio za Ubingwa zipo wazi na hakuna tofauti kubwa ya alama dhidi ya vinara wa Ligi hiyo Young Africans, ambayo jana Jumatatu (Januari 16) ilicheza mchezo wake wa 20 dhidi ya Ihefu FC.
“Hatuwezi kusema kuwa ubingwa ndio basi tena, Michezo bado ipo mingi sana na kuna uwezekano tukafanya vizuri.”
“Tunachotaka ni kupambana hadi mwisho wa msimu ili kuangalia wapi tutakapoishia, lakini lengo kuu ni kumaliza nafasi ya kwanza na kutwaa Ubingwa.” amesema Aggrey Morris ambaye kipindi anacheza Azam FC alitwaa Ubingwa wa Tanzania Bara
Azam FC jana Jumatatu (Januari 16) iliifunga Tanzania Prisons 3-0, katika mchezo wa Mzunguuko wa 20 wa Ligi Kuu Tanzania Bara, Uwanja wa Azam Complex Chamazi jijini Dar es salaam.