Waziri wa Ardhi Nyumba na Maendeleo ya Makazi, Dkt. Angelina Mabula amesema watahakikisha wanaweka mpango bora wa matumizi ya ardhi katika maeneo ambayo yameondolewa katika hifadhi ili wananchi waweze kufanya shughuli zao kimpangilio kwa wakati.
Dkt. Mabula, ameyasema hayo wakati Waziri Mkuu, Kassim Majaliwa alipozungumza na wadau, wawekezaji wa Bonde la Usangu, wakulima wa mpunga, wamiliki wa mashine za kukoboa mpunga na wafugaji Januari 16, 2023 Mkoani Mbeya.
Amesema, pia watahakikisha wananchi hao wanapata hati miliki za maeneo yao ili waweze kuzitumia katika shughuli mbalimbali za maendeleo na mpango wa uandaaji utafanyika kwenye vijiji vyote vinavyohusika.
Akiongea katika Mkoa huo, Waziri Mkuu alisema Serikali imeamua kuitoa nje ya hifadhi ranchi ya Usangu kwa ajili ya shughuli za ufugaji wa kisasa ambapo pia mgogoro wa matumizi ya ardhi Wilayani Mbarali mkoani Mbeya uliodumu kwa miaka 15, uliokuwa ukihusisha wakazi wa Wilaya hiyo katika eneo la Bonde la Usangu dhidi ya hifadhi ya Taifa ya Ruaha, ulimalizwa.