Shirikisho la Soka Amerika ya Kusini ‘COMNEBOL’ limeialika timu ya taifa ya Morocco kushiriki Fainali za Mataifa ya ukanda huo ‘COPA AMERICA 2024’.
Fainali za COPA AMERICA 2024 zimepangwa kuunguruma nchini Ecuador kati ya June-Julai 2024, huku Mabingwa wa Dunia Argentina wakiwa mabingwa watetezi.
Taarifa zinaeleza kuwa matokeo ya kushangaza na kiwango kilichooneshwa na kikosi cha Morocco wakati wa Fainali za Kombe la Dunia 2022, vimewavutia Maafisa wa COMNEBOL na kufikia maamuzi ya kulialika taifa hilo katika Fainali za 48 za COPA AMERICA.
Morocco imekuwa timu ya kwanza kutoka Barani Afrika kufika Nusu Fainali ya Kombe la Dunia, ikivunja rekodi iliyowekwa na mataifa ya Cameroon, Ghana na Senegal yaliyoishia Robo Fainali.
Hata hivyo bado taarifa za mwaliko huo hazijathibitishwa na Shirikisho la Soka nchini Morocco ‘FMRF’ ambalo linapaswa kukubali ama kukataa.
Endapo Morocco itakubali Mwaliko wa ‘COMNEBOL’ itaandika historia mpya katika Soka Dunia kwa kuwa taifa la kwanza kutoka Barani Afrika kushiriki Fainali za COPA AMERICA.