Klabu ya Simba SC imetangaza dhamira ya kurejesha heshima ya Ubingwa wa Kombe la Shirikisho Tanzania Bara ‘ASFC’ ambayo waliipoteza msimu uliopita 2021/22.

Simba SC ilitolewa Nusu Fainali ya ‘ASFC’ kwa kufungwa 1-0 na Young Africans katika Uwanja wa CCM Kirumba jijini Mwanza, na kusitisha ubabe wao kwenye michuano hiyo, ambayo walitawala kwa misimu miwili mfululizo.

Meneja wa Habari na Mawasilino wa Klabu hiyo ya Msimbazi Ahmed Ally amesema, kikosi chao kimekamilisha maandalizi ya mchezo wa kesho Jumamosi (Januari 28) dhidi ya Coastal Union na wana matumaini makubwa ya kuibuka na ushindi.

Amesema Wachezaji wote wameonyesha kuwa tayari kwa mchezo huo, huku kila mmoja akiahidi kuipambania timu kwa ajili ya kuwafurahisha Wanasimba, ambao wametakiwa kufika kwa wingi Uwanja wa Benjamin Mkapa kushuhudia mchezo huo, ambao utaanza saa moja usiku.

“Tunahitaji kuchukua Kombe letu ambalo tulilipoteza kwa bahati mbaya msimu uliopita, kwa hiyo tumefanya maandalizi mazuri yanayoendana na ushindani wa mpinzani wetu.”

“Kikosi kimekamilisha maandalizi ya kuelekea mchezo wetu wa kesho dhidi ya Coastal Union, kila mchezaji ameonyesha kuwa tayari kwa kupambana na kupata matokeo kwa ajili ya Wanasimba, kwa hiyo tunatarajia mkubwa kutoka kwao.” amesema Ahmed Ally

Morocco yaalikwa Copa America 2024
Simba SC yapenyeza makachero Guinea