Shirikisho la Soka Duniani ‘FIFA’ limethibitisha kuwa kwa mara ya kwanza, Waamuzi watakaoamua michezo ya Kombe la Dunia kwa ngazi ya vilabu watawasiliana moja kwa moja na watazamaji wataokuwepo Uwanja na Nyumbani, wakati Waamuzi wakiwa wanatumia msaada ya VAR.
Kupitia mitandao yao ya kijamii ya FIFA, Rais Gianni Infantino amesema watazamaji watakaohudhuria viwanjani na wale wanaotazama kupitia Luninga, watapata fursa ya kuzungumza moja kwa moja na Mwamuzi ambaye yupo uwanjani, atatumia kipaza sauti chake (Microphone) akiwa kwenye VAR.
“Kwa mara ya kwanza, Mwamuzi atazungumza moja kwa moja na mashabiki uwanjani na watazamaji wa Runinga nyumbani kupitia kipaza sauti cha Mwamuzi huyo, akielezea kwa nini uamuzi umefanywa.”
“Hii ni sehemu ya majaribio ya FIFA kwani tunataka kila wakati kuboresha uwazi na ubayana wa VAR na kuboresha elimu. Tunaamini mtaipenda!,” amesema Rais wa FIFA, Gianni Infantino
Infantino amesema kuwa, hatua hiyo itasaidia kuwepo uwazi zaidi juu ya maamuzi ya waamuzi hao. Hata hivyo amesema jaribio hilo litaanza kwenye Michuano ya Kombe la Dunia kwa ngazi ya Vilabu (FIFA Club World Cup) nchini Morocco kuanzia leo Februari Mosi hadi Februari 11, 2023.