Mbunge wa Vunjo, Dkt. Charles Kimei amesema miaka mitano ya James Mbatia na kumi ya Augustino Mrema ya uwepo wao jimbonio haikufanikisha mambo ya kimaendeleo na kwa miaka miwili ya uwepo wa Rais Samia madarakani, umeleta mabadiliko Vunjo inayokaribia kuwa kama Toronto.
Dkt. Kimei ameyasema hayo wakati akifanya mahojiano maalum na Dar24 Media na kuongeza kuwa, mpaka sasa kwa kushirikiana na wananchi wa jimbo lake wamefanya mambo mengi ambayo yalikuwa hayakafanikishwa kwa karibu miaka ishirini.
Amesema, “hawa viongozi hawakuleta maendeleo kwasababu naamini hawakuwa na nia njema, huwezi kuwa Bungeni pale halafu wakati wa kujadili bajeti we unatoka nje, sisi tunakimbizana na Mawaziri kuwaona watusaidie kutatua shida za wananchi mtu yupo nyumbani hufanyi kitu.”
Amesema, kwasasa jimbo la Vunjo ni kama wanaanza upya kwani hata katika miaka mitano ya Hayati Rais Magufuli madarakani hawakuwa na ushirikiano wa kutosha na Serikali na kwamba walijikita zaidi katika mambo ya kiafya na sasa awamu hii imejielekeza katika maendeleo ya Wananchi.