Tetemeko la ardhi lenye kipimo cha 6.4 limewauwa watu watatu na kujeruhi wengine zaidi ya 200 katika baadhi ya maeneo ya Uturuki yaliyoharibiwa na tetemeko jingine kubwa kuwahi kutokea nchini humo wiki mbili zilizopita ambapo watu zaidi ya 45,000 walifariki.
Tetemeko hilo lilisababisha majengo mengine zaidi kuporomoka, na kuwanasa baadhi ya watu, huku ikiripotiwa uwepo wa idadi ya wengi waliojeruhiwa katika nchi jirani ya Syria huku juhudi za uokoaji zikiendelea.
Kitovu cha tetemeko hilo lililotokea Februari 20, 2023 kilikuwa katika mji wa Defne, uliopo mkoa wa Uturuki wa Hatay, eneo ambalo liliathirika vibaya katika tetemeko la Februari 6, 2023 kwa kipimo cha 7.8.
Inarifiwa kuwa, tetemeko hilo pia lilisikika katika nchi ya Syria, Jordan, Cyprus na Misri, likifuatiwa na tetemeko la pili la kipimo cha 5.8, huku Waziri wa mambo ya ndani wa Uturuki Suleyman Soylu akisema watu watatu waliuawa na wengine 213 kujeruhiwa.