Beki wa Vipers SC Juuko Murshid ametamba iwe Mvua iwe Jua, lazima kikosi chao kiibuke na ushindi dhidi ya Simba SC, katika mchezo wa Mzunguuko watatu wa Kundi C, Ligi ya Mabingwa Barani Afrika.

Simba SC ya Tanzania itacheza dhidi ya Vipers SC ya Uganda baadae leo Jumamosi (Februari 25), katika Uwanja wa St. Mary’s-Kitende mjini Entebbe.

Juuko ambaye aliwahi kuitumikia Simba SC kuanzia mwaka 2014–2019, amesema anaitambua klabu hiyo na baadhi ya wachezaji aliocheza nao bado wapo kwenye kikosi cha Mnyama kilichoelekea Uganda, hivyo atatumia uzoefu huo kuisaidia Vipers kushinda.

“Naijua vizuri Simba. Naelewa kuna vitu vimebadilika kwa sasa, lakini sio vyote mfano kuna wachezaji tulicheza nao na hadi sasa wapo kikosini, vivyo hivyo mambo kama falsafa naamini bado ni yaleyale.”

“Ninaamini kwa maandalizi tuliyoyafanya, tuna matumaini makubwa ya kushinda dhidi ya Simba SC, binafsi nipo tayari kupambana na kuisaidia timu yangu kutimiza lengo lake leo.” amesema Juuko Murshid

Hadi sasa kwenye Ligi ya Mabingwa Barani Afrika, Vipers SC imejikusanyia alama moja baada ya kutoka sare ya 0-0 dhidi ya Horoya AC ya Guinea mwishoni mwa juma lililopita, huku Simba SC ikiambulia patupu na kujikuta ikiburuza mkia wa Kundi C.

Abdi Banda aishauri Simba SC Ligi ya Mabingwa
Simba SC yashikili ajira ya Kocha Vipers SC