Aliyewahi kuwa Beki wa Simba SC Abdi Banda, amesema kuna kitu amekiona cha kuisaidia timu hiyo katika michezo iliyosalia ya Kundi C Ligi ya Mabingwa Barani Afrika, baada ya kupoteza dhidi ya Raja Casablanca (Morocco) na Horoya AC (Guinea).

Simba SC leo Jumamosi (Februari 25) inacheza mchezo wa Mzunguuko watatu wa Kundi C dhidi ya Mabingwa wa Uganda Vipers SC itakayokuwa nyumbani katika Uwanja wa St. Mary’s-Kitende mjini Entebbe.

Banda ambaye kwa sasa anacheza soka Afrika Kusini katika klabu ya Chippa United, amesema kuna wajibu wa Wachezaji watakaocheza Safu ya Ulinzi Simba SC katika michezo iliyosalia ya Kundi C, kukumbushana majukumu na kuwasoma wapinzani wao ni hatari kwa mipira gani wanapofika langoni kwao.

Banda ambaye aliichezea Simba SC kuanzia mwaka 2014-2017, kisha alikwenda kujiunga na Baroka FC ya Afrika Kusini mwaka 2017-2019, amesema michuano ya CAF inahitaji mambo muhimu kama nafasi, ulinzi na kufunga.

“Nikitazama kikosi cha Simba SC kina wachezaji wazuri wa kuamua matokeo, kufungwa na Raja Casablanca haimanishi ni wabaya ila ni aina ya timu waliyocheza nayo, ilikuwa kimbinu zaidi, hivyo kupitia mchezo huo yapo mengi wanapaswa wajifunze.”

“Kwenye mchezo wao na Vipers ya Uganda, mabeki wajitahidi kuwa na mawasiliano mmoja akitoka basi wanaobaki lazima wawe makini na miondoko ya wapinzani wao wanapokuwa wanakwenda kwenye lango lao.”

“Kwa upande wa viungo na washambuliaji wanatakiwa kushambulia kulingana na hali ya mchezo husika, mfano timu pinzani ikiwa na wachezaji warefu lazima watacheza mipira ya juu, hivyo inapaswa icheze mpira wa chini na wa moja kwa moja wenye faida.” amesema Banda

Beki huyo ambaye pia amewahi kuitwa kwenye kikosi cha Taifa Stars ameongeza kuwa bado ana imani Simba SC inaweza kufanya mambo makubwa kwenye mchezo unaofuata licha ya kupoteza michezo miwili kwenye hatua hiyo.

Kocha wa Simba SC Roberto Oliveira ‘Robertinho’ ana kazi ngumu ya kuhakikisha angalau anashinda michezo iliyo mbele yake, kwani aliyekuwa anakaimu Juma Mgunda alifanya kitu kwenye michuano hiyo.

Uvamizi Ukraine: Mahakama yataka Putin akamatwe
Juuko Murshid atamba kuisasambua Simba SC