Kamishna wa Polisi Jamii nchini CP. Faustine Shilogile amekutana na viongozi wa Serikali za mitaa kujadili tatizo la mauaji linaloendelea kupoteza nguvu kazi ya Taifa mkoani Kagera.

Akiongea na Watendaji wa Kata, Vijiji, Wakaguzi wa Kata,Viongozi wa Dini, Kamati ya amani pamoja na Wazee wa Mila leo katika ukumbi wa Polisi wilayani Bukoba, Kamishina Shilogile amewakumbusha viongozi hao kuwajibika ipasavyo kwa wananchi wanaowaongoza ili kutatua kero za kihalifu katika maeneo wanayoishi.

Kuhusu suala la mauaji yaliyokithiri Mkoani humo amesema tiba ya tatizo hilo ni viongozi wa Serikali za mitaa, Jeshi la Polisi pamoja na viongozi wa dini kushirikiana kwa pamoja kuhakikisha kuwa wanatoa elimu zaidi juu ya athari za matukio ya mauaji na matukio mengine ya uhalifu ili jamii ibadilike kifikra na kuachana na matukio hayo.

Aidha, katika kikao hicho watoa mada wakiongozwa na Kamishina Msaidizi Mwandamizi wa Polisi, Engelbert Kiondo walitoa elimu kwa kina kuhusu ushirikishwaji wa Jamii katika suala zima la kupambana na uhalifu hasa mauaji, ubakaji na ukatili dhidi ya binadamu na kuwaomba viongozi wote wa Serikali za mitaa wakaendelee kutoa elimu hiyo kwa wananchi katika Kata zao ili kuweza kuzuia uwepo wa matukio hayo.

Kamishna Shilogile pamoja na vipngozi alioambatana nao wanaendelea na ziara yao mkoani Kagera katika wilaya za Missenyi, Muleba na Ngara.

Habari Kuu kwenye magazeti ya leo Machi 2, 2023
Huduma ya maji: Aweso ataka kero za wananchi zitatuliwe