Wakati Simba SC ikitarajiwa kuikabili Mtibwa Sugar kesho Jumamosi (Machi 11) katika mchezo wa Ligi Kuu Tanzania Bara, Kocha Mkuu wa Klabu hiyo ya Msimbazi Roberto Oliveira ‘Robertinho’ anaendelea kuumiza kichwa kutokana na safu yake ya ushambuliaji kusumbuliwa na ubutu wa kutumia nafasi wanazotengeneza.

Simba SC ilinusurika kupoteza dhidi ya Azam FC katika mchezo wa Ligi Kuu mwezi uliopita, lakini ikaonesha udhaifu kwa kushindwa kutumia nafasi inazozitengeneza katika lango la wapinzani, ilipocheza dhidi ya Vipers SC kwenye michuano ya Ligi ya Mabingwa Barani Afrika.

Mchezo dhidi ya Azam FC Simba SC iliambulia sare ya 1-1, huku bao la kusawazisha likipatikana kwa Beki wa timu pinzani kujifunga kwa kushindwa kuukowa sawasawa mpira uliopigwa na Kibu Denis.

Kwenye Michuano ya Kimataifa Simba SC imekuwa ikipata ushindi wa bao moja Katika hatua ya makundi ya Ligi ya Mabingwa Afrika msimu huu, Simba ikiwa kundi C, imetupia mabao mawili ndani ya dakika 360.

Kwenye mabao hayo, wafungaji ni beki Henock Inonga na kiungo Clatous Chama, wote wakifunga dhidi ya Vipers ugenini na nyumbani.

Ikumbukwe kuwa, washambuliaji wa Simba ni Jean Baleke, Moses Phiri, John Bocco na Habib Kyombo ambao bado hawajafunga.

Ukuta wa Simba umeruhusu mabao manne kwenye michezo minne ya michuano hiyo hatua ya Makundi, huku ikicheza michezo miwili bila ya kuruhusu bao.

kutokana na tatizo hilo Kocha Robertinho amesema: “Unajua huwezi kupata alama tatu ikiwa hautafunga, washambuliaji wangu wamekuwa na tatizo hilo la kufunga, lakini tunalifanyia kazi.”

“Inabidi ujue kwamba mashindano haya ya CAF ni magumu na hata kwenye Michezo ya Ligi Kuu, nasi tunapambana kufanya vizuri kwa wachezaji wote kufunga. Tunatengeneza nafasi nyingi kwenye kila mchezo, lakini kuzitumia hapo ni tatizo.”

Simba SC tayari imeshawasili mkoani Morogoro tangu jana Alhamis, na leo Ijumaa itaelekea Manungu wilayani Mvomero tayari kwa mchezo dhidi ya Mtibwa Sugar utakaopigwa Uwanja wa Manungu Complex.

Kisa Sigara: Aachwa na mumewe, aapa kutovuta tena
Young Africans yapandisha kiburi Ligi Kuu