Uongozi wa KMC FC umesema utahakikisha michezo mitano iliyobaki katika Ligi Kuu Bara msimu huu 2022/23, timu yao inacheza kama fainali ili kufanikisha usalama wa kuendelea kusalia katika Ligi hiyo kwa msimu ujao wa 2023/24.
Timu hiyo ya Manispaa ya Kinondoni yenye maskani yake Dar es Salaam, ipo kwenye mapumziko ya muda wa siku 10 kwa kuwa hawatakuwa na mchezo wowote hadi Aprili 10, mwaka huu baada ya Alhamisi iliyopita kuichapa Kagera Sugar mabao 2-0.
Afisa Habari wa KMC FC Christina Mwagala amesema wanatambua wapo kwenye wakati mgumu, lakini watapambana michezo iliyobaki wawe salama.
“Tuna kazi kubwa ya kufanya kutokana na michezo iliyopo ipo pamoja na nafasi ambayo tupo, michezo iliyobaki itakuwa ni kama Fainali, tunaamini kwamba tutapata matokeo mazuri.
“Ushindi wetu dhidi ya Kagera Sugar unatufanya tuwe kwenye nafasi nzuri kwa kupata alama tatu, kazi inazidi kuwa imara, hivyo mashabiki wazidi kuwa pamoja nasi,” amesema Mwagala.
KMC ipo nafasi ya 12 kwenye msimamo wa Ligi Kuu Tanzania Bara ikiwa na alama 26 baada ya kucheza michezo 25.
Michezo mitano iliyobaki ni dhidi ya Geita Gold (nyumbani), Dodoma Jiji (ugenini), Singida Big Stars (nyumbani), Prisons (ugenini) na Mbeya City (ugenini).