Uongozi wa Simba SC umekanusha taarifa za kuwa katika mipango ya kumsajili Kiungo wa AS Real Bamako ya Mali, Ibourahima Sidibé ambaye pia anahusishwa na Mabingwa wa Soka Tanzania Bara Young Africans.
Sidibe ni kati ya viungo hatari zaidi kutokea ukanda huo wa Magharibi ambapo alijiunga na AS Real Bamako misimu mitatu iliyopita na aliwahi pia kwenda kwa mkopo katika moja ya klabu ya nchini Saudi Arabia. Nyota huyo ambaye anatumia zaidi mguu wa kushoto anamudu kucheza nafasi za winga zote na kiungo mshambuliaji.
Taarifa zinaeleza kuwa, tangu Klabu za Simba SC na Young Africans, zishuhudie uwezo wa kiungo huyo zimejikuta zikiviziana namna ya kuhakikisha wanamalizana naye kabla ya kutua kwenye meza ya mazungumzo na klabu yake hiyo.
Meneja wa Habari na Mawasilino wa Simba SC Ahmed Ally amesema ni mapema mno kwao kuanza kufikiria usajili wa Wachezaji katika kipindi hiki, kwani wapo katika majukumu ya kuliwakilisha Taifa kwenye Michuano ya Ligi ya Mabingwa Barani Afrika.
Ahmed amesema, suala la kuhusishwa na tetesi za usajili ni la kawaida, lakini Uongozi wao upo katika harakati za kuhakikisha timu yao inafanya vizuri na kuingia Hatua ya Robo Fainali na ikiwezekana Nusu Fainali Ligi ya Mabingwa Barani Afrika.
“Ngoja nikwambie, usajili haujafunguliwa lakini kwa sasa viongozi wote ndani ya Simba SC tunatakiwa kufuatilia kila michezo ya Kombe la Shirikisho Barani Afrika, hadi wawe sawa,”
“Sisi hatutasajili wachezaji wa aina hiyo, huyo Sidibe ni mchezaji mzuri lakini kwa sasa sina taarifa za moja kwa moja kama atasajiliwa au laa, tusubiri usajili ufunguliwe.” Amesema Ahmed Ally
Ibourahima Sidibé alianza kucheza soka la ushindani mwaka 2013 akiwa na klabu ya Djoliba AC (Mali) na baadae alisajiliwa AS Real Bamako (2013–2014).
Kati ya mwaka 2014–2017 alisajiliwa MAS Fez 42 ya Morocco ambayo aliitumikiwa katika michezo 42 na kufunga mabao matatu, na baadae alisajiliwa FUS Rabat (2017–2019), kabla ya kusajiliwa kwa mkopo Kawkab Marrakech (2018–2019).
Mwaka 2019 aliamua kurejea nyumbani Mali na kusajiliwa tena na AS Real Bamako ambayo anaendelea kuitumikia hadi sasa.