Mfuko wa Taifa wa Bima ya Afya -NHIF, umefafanua kuwa kufanya maboresho ya utaratibu wa usajili na huduma kwa watoto waliokuwa wanasajiliwa kupitia utaratibu wa Bima ya Afya ya Toto Afya Kadi kwa lengo la kuwafikia watoto wengi walio nje ya huduma.
Kwa mujibu wa Mtendaji Mkuu wa NHIF, Bernard Konga imeeleza kuwa, wazazi au walezi wanashauriwa kuwasajili watoto wao kama wategemezi wao wa Bima ya Afya au kusajili kupitia shule wanazosoma.
Amesema, hatua itasaidia kuongeza wigo wa wanachama katika mfumo wa bima ya afya kuelekea bima ya afya kwa wote, na kuhakikisha wanachama katika makundi hayo wanajiunga kama familia, kaya na makundi ya wanafunzi kwa shule wanazosoma.
“Mpango wa Toto Afya Kadi ulianza mwaka 2016 ikiwa na lengo la kuwafikia kundi kubwa la watoto walio chini ya miaka 18 ambao kitakwimu ni zaidi ya nusu ya wananchi wote ili kufikia azma ya serikali ya watu wote kuwa na bima ya afya,” amesema Konga.
Aidha, Konga amebainisha kuwa, tangu kuanza kulihudumia kundi la watoto kwa kipindi cha miaka saba sasa, mfuko umefikia watoto 210,664 walio chini ya miaka 18 na kwamba NHIF imekuwa ikishirikiana na shule za msingi na sekondari ili kusajili wanafunzi kunufaika na bima ya afya.
Hata hivyo, kundi la watoto watakaokosa sifa na vigezo vya kuandikishwa kupitia bima za wazazi kwa mwajiri au vifurushi wajiandikisha kupitia vyuo, shule au vituo rasmi vya kuelekea watoto waishio katika mazingira magumu.