Kiungo kutoka nchini Nigeria na Klabu ya Simba SC Victor Akpan ameingilia kati sakata la Kiungo kutoka Zanzibar Feisal Salum ‘Fei Toto’ na Uongozi wa Klabu ya Young Africans, ambalo limechukua nafasi kubwa katika medani za soka la Bongo.
Pande hizo mbili zinasigana katika sakata la kuvunjwa kwa mkataba uliopo baina yao, huku Mchezaji akihitaji kuondoka Young Africans baada ya kuthibitisha hilo mwishoni mwa mwaka 2022, huku Uongozi wa klabu hiyo ukisisitiza utaratibu kufuatwa.
Akpan ambaye kwa sasa anaitumikia klabu ya Ihefu FC kwa mkopo amesema hajashangazwa na kinachoendelea baina ya Feo Toto na Uongozi wa Young Africans, kwani anachoamini maisha ya mchezaji yanategemea kipato anachokivuna wakati wakicheza soka.
Amesema hata kama Fei Toto amekosea kudai haki yake kwa utaratibu, bado anapaswa kuheshimiwa kwa sababu ameonesha kujitambua kwa kutumia uwezo wake kisoka, ambao unatakiwa kumuingizia kipato kutokana na thamani alionayo.
“Kuhusu Fei Toto, mimi kama mchezaji ninayejua mchezo wa mpira ni wa muda mfupi naelewa anachopitia, wanaomshangilia leo akiwa staa watamcheka akistaafu kama hatajiwekeza kimaisha.”
“Huenda kweli kakosea kuvunja mkataba, lakini Yanga wanaionaje thamani ya Fei Toto maana kwa sasa yupo kwenye kiwango cha juu asipopewa anachokitaka atapewa nyakati zipi, soka lina mambo mengi sana.” Amesema Akpan
Mara mbili mfululizo Feisal Salum ‘Fei Toto’ amekwama mbele ya Kamati ya Sheria na Hadhi za Wachezaji ya TFF akitakiwa kurejea kambini kujiunga na wenzake, kutokana na kubainika mkataba uliopo dhidi ya Young Africans ni halali.