Kocha Mkuu wa Simba SC Roberto Olivieira ‘Robertinho’ amewarejesha kambini wachezaji wa klabu hiyo, tayari kwa maandalizi ya mchezo wa Mzunguuko wasita wa Kundi C, Ligi ya Mabingwa Barani Afrika dhidi ya Raja Casablanca.

Simba SC itacheza ugenini mjini Casablanca April Mosi, huku ikiwa na uhakika wa kucheza Robo Fainali Ligi ya Mabingwa Barani Afrika, ikiwa na alama 09, ikitanguliwa na Raja Casablanca yenye alama 13.

Kocha Robertinho aliwataka Wachezaji wake wote ambao hawajaitwa kwenye majukumu ya timu za taifa kurejea kambini jana Alhamisi (Machi 23) kuanza rasmi maandalizi ya mchezo huo.

Simba SC itaingia katika mchezo huo ikiwa na kumbukumbu ya kipigo cha mabao 3-0 kwenye mchezo wa Mzunguuko wapili wa kundi C uliopigwa Uwanja wa Benjamin Mkapa, jijini Dar es Salaam.

Meneja wa Habari na Mawasiliano wa Simba, Ahmed Ally amesema: “Baada ya ushindi mzito wa mabao 7-0 dhidi ya Horoya na kufuzu hatua ya Robo Fainali ya Ligi ya Mabingwa Afrika wachezaji wetu walipewa mapumziko ya siku nne na walirejea kambini jana Alhamis na leo Ijumaa (Machi 24) wanaanza maandalizi ya mchezo dhidi ya Raja Casablanca.”

“Licha ya tumefuzu Robo Fainali, tunafahamu huu itakuwa mchezo mgumu kwetu lakini tunataka kupambana kwa ajili ya heshima ya Simba SC.”

Kocha Coastal Union matumaini kibao safari ya Dodoma
Southgate: Ninaimani kubwa na Harry Kane