Kikosi cha Coastal Union ya Tanga kimeanza mazoezi rasmi ya kujiandaa na mechi zao zilizobaki za Ligi Kuu Bara baada ya mapumziko ya takribani wiki moja.
Ikumbukwe kuwa baada ya mchezo wa Ligi Kuu Tanzania Bara dhidi ya Singida Big Star ambao ulichezwa Machi 12, katika Uwanja wa Mkwakwani na kumalizika kwa sare ya 1-1 katika Uwanja, Kocha wa Wagosi hao wa Kaya, Fikiri Elias, aliwapa vijana wake mapumziko na sasa wamerejea kambini kujiandaa na michezo mingine ya ligi hiyo.
Coastal Union ambao kwenye msimamo wa Ligi Kuu wapo nafasi ya 13 wamebakiza michezo mitano ambapo mchezo uliopo mbele yao ni dhidi ya Dodoma Jiji utakaochezwa Aprili 9 katika Uwanja wa Jamhuri mjini Dodoma.
Kocha Elias amesema: “Baada ya mapumziko tumerejea na kibarua kilichopo mbele yetu ni kujiandaa na mchezo wetu dhidi ya Dodoma.
“Utakuwa mchezo mgumu sana kwetu kutokana na nafasi tuliyopo kwa sasa, hivyo tunapaswa kujiandaa vizuri.”
Michezo mingine ambayo wamebakiza Coastal Union ni dhidi ya Mtibwa Sugar, Ihefu FC, Azam FC ambayo yote watakuwa nyumbani na mchezo wa mwisho watacheza dhidi ya Simba SC jijini Dar es salaam.