Mkurugenzi wa Idara ya Menejimenti ya Maafa Ofisi ya Waziri Mkuu, Meja Jenerali Charles Mbuge ametaka kuanzishwa kwa timu Mtambuka ya Wataalam ya kukabiliana wa Maafa kila Mkoa, ambayo itarahisisha mawasiliano ya ndani wakati wa kukabiliana na dharura.
Meja Jenerali Mbuge, ameyasema hayo wakati akifungua Kikao kazi cha kuweka mkakati wa kuanzisha timu ya Wataalam ya kukabiliana na maafa Mkoa wa Dodoma (Dodoma Mult Agency Emergency Response Team – DoMAERT), kilichofanyika Jijini Dodoma.
Amesema, uwepo wa timu hiyo pia itasaidia kuunganisha nguvu kwa wadau waliopo ndani ya Mkoa na kuweza kutumia rasilimali zilizopo kuhakikisha maafa yanakabiliwa na wananchi kuwa katika mazingira salama.
“Nchi yetu imekuwa ikipata maafa ambayo uratibu wake unahitaji kila Mkoa kuwa na timu mtambuka ya Wataalam ya kukabiliana wa maafa kwa mujibu wa Sheria ya Usimamizi ya Maafa Na. 6 ya mwaka 2022 na kanuni zake, hivyo uundwaji wa timu hizo ni muhimu kwa usalama wa wananchi na mali zao,” amesema Mbuge.
Katika hatua nyingine, Meja Jenerali Mbuge amesema Idara ya Menejimeti ya Maafa Ofisi ya Waziri Mkuu imeendelea kuchukua hatua za kupunguza madhara, kwa kuhakikisha usimamizi na uratibu wa maafa na huduma za dharura zinatolewa kwa wakati na kuzingatia mipango, miongozo na mikakati ya kitaifa na kisekta.
Amesema, “Idara ya Menejimenti ya Maafa kwa kuzingatia Sera ya Taifa ya Usimamizi wa Maafa ya Mwaka 2004 na Sheria ya Usimamizi wa Maafa, Na. 6 ya mwaka 2022 inaratibu na kusimamia masuala ya maafa nchini.”