Baada ya kupoteza matumaini ya kutwaa taji la Ligi Kuu Bara msimu huu 2022/23, Azam FC imehamishia nguvu zake kwenye Michuano ya Kombe la Shirikisho Tanzania Bara ‘ASFC’.
Aprili 3, mwaka huu, Azam FC itakuwa na kibarua cha kuikabili Mtibwa Sugar, ukiwa ni mchezo wa hatua ya Robo Fainali ya michuano hiyo unaotarajiwa kuchezwa Uwanja wa Azam Complex, jijini Dar es salaam.
Afisa Habari wa Azam FC, Hasheem Ibwe, alisema kuwa wanatambua umuhimu wa mashindano hayo na kila kitu kipo vizuri, hivyo kikosi chao kimejipanga kupata ushindi dhidi ya Mtibwa Sugar na kusonga mbele.
“Timu kubwa inafanya vitu vikubwa na kupata matokeo mazuri kwenye michezo yake, hivyo nasi tunajipanga kufanya mambo makubwa kwa kupata matokeo mazuri.
“Safari hii tumedhamiria kufanya kweli kwenye Kombe la Azam Sports Federation, ndio maana tulianza kupata ushindi mkubwa kwenye michezo ile ya mwanzo, ikumbukwe tuliwafunga Malimao mabao mengi,” amesema Ibwe