Jenerali, Muhoozi Kainerugaba, mtoto wa Rais wa Uganda, Yoweri Museveni ametangaza kuwa nchi yake itatuma wanajeshi, ili kuulinda mji wa Moscow, ikiwa utakabiliwa na tishio.
Jenerali Muhoozi ambaye ni mfuasi wa Rais wa Urusi, Vladimir Putin ameyasema hayo Machi 30 2023 na kuongeza kuwa nchi za magharibi zinapoteza muda wake na propaganda zisizo na maana za kuiunga mkono Ukraine.
“Niite mfuasi wa Putin ukipenda, lakini sisi, Uganda tutatuma wanajeshi kuilinda Moscow ikiwa itatishiwa na mabeberu, “ aliandika Muhoozi Kainerugaba kwenye ukurasa wake wa Twitter.
Aidha, Kainerugaba ambaye amepata umaarufu mkubwa kutokana na maoni yake juu ya mambo mbalimbali, mapema mwezi huu alitangaza kwamba anapanga kuwania urais kwenye uchaguzi wa 2026 akidai kuwa Wazee sasa wanatakiwa kupumzika.
Juzi (Machi 29, 2023), Muhoozi pia alitangaza kuwa ataanzisha kituo cha Televisheni na Radio chini ya chapa yake ya MK, huku akidai kuwa moja ya maeneo ya kwanza atakayoyatembelea itakuwa ni Russia.